2 Kings 17

Hoshea, Mfalme Wa Mwisho Katika Israeli

1 aKatika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Ahazi mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, akatawala kwa miaka tisa. 2 bAkafanya maovu machoni pa Bwana, lakini si kama wafalme wengine wa Israeli waliomtangulia.

3 cMfalme Shalmanesa wa Ashuru akainuka dhidi ya Mfalme Hoshea, ambaye hapo mbeleni alikuwa mtumwa wake na kumlipa ushuru. 4 dLakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri, naye hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumtia gerezani. 5Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuizunguka kwa majeshi miaka mitatu. 6 eKatika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawaweka huko Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi.

Israeli Inakwenda Uhamishoni Kwa Sababu Ya Dhambi

7Yote haya yalitokea kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya Bwana Mwenyezi Mungu wao, ambaye alikuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine 8 fna kufuata desturi za mataifa ambayo Bwana alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta. 9 gWaisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya Bwana Mwenyezi Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye maboma walijijengea wenyewe mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote. 10 hWakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda. 11Wakafukiza uvumba kila mahali palipoinuka, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo Bwana alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha Bwana. 12 iWakaabudu sanamu, ingawa Bwana alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.” 13 j Bwana akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na sheria yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu manabii.”

14Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumtegemea Bwana Mwenyezi Mungu wao. 15 kWalizikataa amri zake, na agano alilokuwa amelifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu zisizofaa, nao wenyewe wakawa hawafai. Wakayaigiza mataifa yaliyowazunguka, ingawa Bwana alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya,” nao wakafanya mambo ambayo Bwana alikuwa amewakataza wasifanye.

16 lWakayaacha maagizo yote ya Bwana Mwenyezi Mungu wao na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali. 17 mWakawatoa kafara wana wao na mabinti zao katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa Bwana, wakamghadhibisha.

18Basi Bwana akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki; 19na hata hivyo nao Yuda hawakuzishika amri za Bwana Mwenyezi Mungu wao. Wakafuata desturi ambazo Israeli walikuwa wamezianzisha. 20Kwa hiyo Bwana aliwakataa watu wote wa Israeli; akawatesa na kuwaachia katika mikono ya wateka nyara hadi alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake.

21 nAlipokwisha kuwatenga Israeli mbali na nyumba ya Daudi, wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme wao. Yeroboamu akawashawishi Israeli waache kumfuata Bwana na akawasababisha kutenda dhambi kuu. 22Nao Israeli wakadumu katika dhambi zote za Yeroboamu mwana wa Nebati, nao hawakuziacha 23 ohadi Bwana alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake, kama vile alivyokuwa ameonya kupitia watumishi wake wote manabii. Hivyo watu wa Israeli wakaondolewa kutoka nchi yao kwenda uhamishoni Ashuru, nao wako huko mpaka sasa.

Samaria Inakaliwa Tena

24 pMfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria badala ya Waisraeli. Wakaimiliki Samaria na kuishi katika miji yake. 25 qWakati walianza kuishi humo, hawakumwabudu Bwana, kwa hiyo akatuma simba miongoni mwao, wakawaua baadhi ya watu. 26Habari ikapelekwa kwa mfalme wa Ashuru, kusema: “Watu uliowahamisha na kuwaweka katika miji ya Samaria hawajui kile Mungu wa nchi hiyo anachokitaka. Ametuma simba miongoni mwao, ambao wanawaua, kwa sababu watu hawajui anachokitaka.”

27Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru hivi: “Mtwae mmoja wa makuhani uliowachukua mateka kutoka Samaria ili arudi kuishi humo na awafundishe watu kile ambacho Mungu wa nchi anataka.” 28Basi mmoja wa makuhani ambaye alikuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli na kuwafundisha jinsi ya kumwabudu Bwana.

29 rHata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka mahali pa ibada za miungu ambapo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu. 30Watu kutoka Babeli wakamtengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakamtengeneza Nergali, na watu kutoka Hamathi wakamtengeneza Ashima; 31 sWaavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki, nao Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu. 32 tWalimwabudu Bwana, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu pa ibada. 33Walimwabudu Bwana, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka.

34Mpaka leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu Bwana wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo Bwana aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli. 35 uWakati Bwana alipofanya Agano na Waisraeli, aliwaamuru akisema: “Msiiabudu miungu mingine yoyote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu. 36 vBali imewapasa kumwabudu Bwana aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu na kwake yeye mtatoa dhabihu. 37 wImewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine. 38 xMsisahau agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine. 39Bali, mtamwabudu Bwana Mwenyezi Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.”

40Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali. 41 yHata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu Bwana, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Mpaka leo watoto wao na watoto wa watoto wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.
Copyright information for SwhKC